Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alitoa neno zito! Ingawa ni maoni yake lakini kusema kweli masihara mengine si mazuri.
Mrema alisema hakuna ubaya Rais Jakaya Kikwete akiachwa aongoze nchi kwa muda (zaidi ya Oktoba mwaka huu) ili akamilishe mchakato wa Katiba Inayopendekezwa pamoja na Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Hakuna ubaya wowote kwa Rais Kikwete kuondoka madarakani kabla ya Katiba Mpya kupatikana, si ajabu wala si dhambi. Chambilecho mwenyewe (Kikwete) masuala ya wafanyakazi aliyokuwa hajakamilisha kuyashughulikia, yatashughulikiwa na rais ajaye. Hivyo hata masuala ya Katiba yaliyokuwa hayajamalizika, yatamalizwa na rais ajaye.
Hiyo ndiyo dhana ya kupokezana vijiti, kwani miaka 10 mtu hawezi kukamilisha yote, atafanya ya kiasi chake, mengine atamwachia mwenzake. Anachofanya Mrema ni kumdodesha Kikwete ili atamani kuendelea.
Athari ya kuendelea madarakani sote tunaijua, mfano uko machoni mwetu, nchi jirani ya Burundi, Pierre Nkurunzinza anatamani aendelee kubaki madarakani, kinachotendeka Burundi hivi sasa, tuombe tuendelee kukisikia hivyo hivyo na kukiona kwenye luninga kwani ukweli utakapodhihiri kwetu, si taswira nzuri ya kuiangalia machoni au kuwa ndiyo hali iliyokukabili, huna pa kukimbilia, ni zahama isiyo kifani.
Leo hii kwetu kuna mgomo wa mabasi na daladala tu, kizaazaa hakisemeki, sasa tusiombe kwenda kuyaona ya vurugu za kisiasa na utumiaji wa nguvu za dola.
Watanzania wa leo labda niseme wameerevuka au wameelimika kisiasa, wanazijua haki zao na hata wajibu wao, si wakati tena wa kufuata upepo kama bendera. Watu sasa wanahoji, wanajadili, wanadahala na wanadadavua kwa kina, hawana tena masihara na maisha yao, kwani siasa ndiyo maisha.
Miaka mitano unayompa mtu akuamulie mustakabali wako wa maisha si kitu cha mchezo hata kidogo, ni lazima watu wawe makini, waache tabia ya kuherereza; eti madhali hujamaliza kushughulikia Katiba Mpya, endelea kwa muda kidogo! Dah! balaa hiyo, haiwi hivyo, si katika mipangilio yake, si jambo la kulifanyia masihara hata kidogo.
Jambo la kulisimamia sasa ni kuhakikisha Daftari la Kudumu la Wapigakura linapatikana. Jaji Damian Lubuva ahakikishe mashine za utambulizi wa alama za binadamu (BVR) zinapatikana zote 7,750 zilizopangwa kupatikana na zoezi la uandikishaji linafanyika kwa ufanisi wa kutosha kwa miezi hii mitano iliyosalia.
Ingawa wenzetu Kenya walikuwa na BVR 15,000 kwa watu milioni 14 na wameandikisha kwa siku 50, sisi tuna BVR 7,750 kwa watu milioni 24 lakini huenda tukaandikisha kwa miezi 6. Potelea pote, tunachotaka sisi tuandikishwe tu.
Penye nia, ipo njia, miezi mitano si haba kama Jaji Lubuva na watu wake watajipanga vyema. Ni wazi kuwa hivi sasa wameshatambua changamoto zote za BVR tokea Desemba mwaka jana walipofanya uandikishaji wa majaribio na baadaye Februari 23 mwaka huu kuanza uandikishaji katika mkoa wa Njombe ambao ulichukua mwezi mzima.
Wakati wa uandikishaji wa majaribio, Jaji Lubuva alijinasibu kuwa uandikishaji umefanikiwa katika maeneo ya Kawe, Kilombero na Mlele (Katavi). Walipofika Njombe, BVR zikakataa kusoma alama za vidole sugu, vigumu, vilivyopoteza alama kutokana na kazi ngumu.
No comments:
Post a Comment