Friday, 15 May 2015

Raisi Kikwete awashukia vigogo Kinondoni


SHARE BOOKMARKPRINTEMAILRATING

Rais Jakaya Kikwete akitazama maji yaliyofurika kwenye makazi wa watu eneo la Tegeta, alipofanya ziara ya kuangalia maeneo yaliyoathirika kwa mvua wilayani Kinondoni, jana. Picha na Freddy Maro. 
Na Raymond Kaminyoge

Posted  Ijumaa,Mei15  2015  saa 10:26 AM
KWA UFUPI
Akiwa katika ziara iliyochukua saa moja na nusu katika eneo la Tegeta na Mkwajuni wilayani Kinondoni jana, Rais Kikwete aliwakemea watendaji wa halmashauri hiyo kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka kuyaondoa maji kwenye nyumba hizo.
SHARE THIS STORY
 
 
 
0
Share
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amewashukia watendaji wa Wilaya ya Kinondoni kwa kushindwa kuondoa maji yaliyozingira makazi ya watu eneo la Tegeta Basihaya, Dar es Salaam.
Akiwa katika ziara iliyochukua saa moja na nusu katika eneo la Tegeta na Mkwajuni wilayani Kinondoni jana, Rais Kikwete aliwakemea watendaji wa halmashauri hiyo kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka kuyaondoa maji kwenye nyumba hizo.
“Ninawataka viongozi na watendaji wa Manispaa ya Kinondoni kuyaondoa maji ya mafuriko yaliyozingira nyumba zaidi ya 200… kuyaacha maji hayo hadi sasa ni uzembe.
“Maisha lazima yaendelee kwa wakazi hawa, mafuriko yamewakumba wananchi wetu lakini tangu mvua ianze wiki mbili zilizopita watendaji na wahandisi hamjachukua hatua ya kuyaondoa maji haya ili watu waendelee kuishi,” alisema.
Kwa wiki mbili, mvua zinazoendelea kunyesha, watu 12 wameripotiwa kufa kutokana na mafuriko huku mamia wakiyahama makazi yao.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, Meya wa Manispaa Yusuph Mwenda, watendaji na wakazi wa eneo hilo, Rais Kikwete alisema: “Kuanzia sasa naagiza maji haya yaondolewe ili wananchi warudi kwenye makazi yao. Wahandisi mnafahamu namna ya kuyaondoa, tumieni elimu yenu ya uhandisi kuyaondoa.”
Baada ya kuwasili Tegeta Basihaya saa 6.00 mchana, Rais Kikwete alionyeshwa na Makonda nyumba zilizozingirwa na maji huku akimweleza kuwa wana mpango wa kuweka mifereji itakayoondoa maji hayo na kwamba Sh3 bilioni zinahitajika kwa kazi hiyo.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema: “Nguvu kubwa ielekezeni kuyaondoa maji hayo baada ya hapo mtakaa kupanga namna ya kuweka mifereji ili kuzuia mafuriko hapo baadaye, hakuna sababu za kuanza kujadili bajeti hapa.”
Alisema ili mafuriko katika eneo hilo yasiweze kurudia tena katika miaka ijayo, ni lazima baadhi ya nyumba zibomolewe ili kupisha maeneo ya kuweka mifereji hiyo.
“Mimi si mhandisi lakini hapa ni lazima baadhi ya nyumba zibomolewe ili mtengeneze miundombinu ya kupitisha maji vinginevyo kila mwaka kutakuwa na mafuriko.”
Akiwa katika Bonde la Mkwajuni, Rais Kikwete alisema Serikali itatoa viwanja kwa wakazi wa mabondeni watakaoamua kuhama ili kujiepusha na maafa ambayo yamekuwa yakitokea kila mwaka... “Serikali itawapa viwanja watakaohama mabondeni, nawashauri mhame, haya maisha ya kuishi kwa wasiwasi kila mwaka si mazuri.”
Alisema wananchi hao wanajirudisha nyuma kiuchumi kwa sababu wamekuwa wakipoteza vifaa vyao kwenye mafuriko hayo... “Mwaka huu unanunua vifaa vyako lakini vinakuja kuchukuliwa na mafuriko, maisha gani haya ya shida kila mwaka.”

No comments:

Post a Comment