Friday, 15 May 2015

Ile Picha ya Shilole akiwa wazi sehemu za juu za mwili wake,imesababisha Basata kutoa kauli hii….


shishiSiku chache zikiwa zimepita tangu picha ambayo ilimuonyesha msanii Shilole kuwa wazi baadhi ya sehemu zake za juu akiwa stejini nchi ya Ubeligiji,Mei 14 Baraza la sanaa Tanzania(Basata) wameamua kutoa taarifa yao ambayo imetolewa na Katibu MkuuGodfrey Mngereza,mtu wako wa nguvu barua hiyo imenifikia naomba kushare na wewe.
BASATA YALAANI TABIA CHAFU NA ISIYO NA MAADILI ILIYOONESHWA NA MSANII SHILOLE KWENYE ONESHO LAKE NCHINI UBELIGIJI
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini limeona picha chafu na zisizo na maadili za Msanii Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole alipokuwa akifanya onesho lake nchini Ubeligiji hivi karibuni.
Katika picha hizo ambazo zimelaaniwa na watanzania wengi nchini kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, Shilole anaonekana akiwa Jukwaani huku viungo vyake vya sehemu za siri vikiwa hadharani na zaidi akionesha tabia ambazo kwa kiasi kikubwa zimefedhehesha na kuidhalilisha sekta ya Sanaa na Taifa kwa ujumla.
Aidha, BASATA limepokea malalamiko kwa njia ya simu na mawasiliano ya internet kutoka kwa watanzania waishio ughaibuni wakilaani tukio la Msanii huyo. Katika mawasiliano yao wameeleza kwamba wamefedheheshwa na kudhalilika na tabia hiyo chafu iliyooneshwa na msanii huyu.
Ikumbukwe kwamba, Shilole ni msanii aliyesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa, hivyo anapokwenda nje ya nchi kabla hajapata visa anapewa barua ya utambulisho kama msanii wa Tanzania, hivyo anapokuwa nje ya nchi anatambuliwa kama msanii Mtanzania, anapofanya kinyume na misingi ya kazi ya Sanaa, anajifedhehesha yeye mwenyewe, kazi ya Sanaa na nchi yetu pia.
Aidha, ikumbukwe kwamba BASATA limeshapata kumwita na kumuonya msanii huyu kutokana na tabia yake ya kutokujiheshimu pale awapo jukwaani na yeye aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo chafu. Kwa hiyo kuendelea kwake kufanya matukio hayo na kwa sasa katika ardhi ya nchi nyingine ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na kuiheshimu Sanaa kama kazi nyingine.

BASATA linapenda kueleza kwamba;
  1. Litamuita kwa mara nyingine tena kumtaka ajieleze kwa nini alifanya onesho hilo la kujidhalilisha na kudhalilisha hadhi ya mwanamke, msanii na Sanaa kwa ujumla
  2. Kama maelezo yake hayataridhisha hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake maana tayari ameshadhihirisha kwamba akifanyacho si Sanaa na hakina uhusiano na kazi ya Sanaa ambayo ina heshima yake na inahitaji ubunifu, weledi na kujitambua
BASATA linawakumbusha wasanii wote nchini kuwa Sanaa ni kazi kama kazi zingine lakini siku za hivi karibuni wasanii wengi wamekuwa wakikiuka suala zima la maadili kwa kutengeneza kazi chafu zisizofaa mbele ya jamii ya watanzania wanaoipenda na kuiheshimu kazi ya Sanaa yenye staha. Tuungane kwa pamoja kukemea kazi chafu zinazozalishwa na wasanii wasiojitambua kwani suala la maadili ni suala mtambuka na linaanzia katika ngazi ya familia.
Aidha, BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara wanapopata mialiko ya kikazi kwenda nje ya nchi. Linawakumbusha kwamba haiwezekani msanii kutumia picha chafu na mavazi dhalili na kuonyesha utupu katika kuvuta mashabiki.

No comments:

Post a Comment