Wednesday, 6 May 2015

Bei ya Petroli yazidi kupaa

Machi 3, petroli ilishuka kwa kiwango kikubwa katika kipindi kirefu nchini ilipofikia Sh1,652 baada ya mafuta ghafi katika soko la dunia kuporomoka kwa zaidi ya nusu ya bei yake na kufikia Dola 48 za Marekani kwa pipa. Kwa sasa bei ya mafuta ghafi kwenye soko la dunia imepanda na kufikia Dola 60 kwa pipa.   

Dar es Salaam. Bei ya petroli imeendelea kushika kasi ya kupanda tangu ilipopungua kwa kiasi kikubwa mwezi Februari baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza ongezeko la Sh111 wakati dizeli ikipanda kwa Sh23.
Machi 3, petroli ilishuka kwa kiwango kikubwa katika kipindi kirefu nchini ilipofikia Sh1,652 baada ya mafuta ghafi katika soko la dunia kuporomoka kwa zaidi ya nusu ya bei yake na kufikia Dola 48 za Marekani kwa pipa. Kwa sasa bei ya mafuta ghafi kwenye soko la dunia imepanda na kufikia Dola 60 kwa pipa.
Bei ya juu ya petroli ilikuwa Desemba mwaka jana ilipofikia Sh2,266 kabla ya kushuka Januari 2015 kwa Sh311 na kufikia Sh1,955.
Kwa mujibu wa viwango vilivyotangazwa jana na Ewura, bei ya petroli imepanda kutoka Sh1,755 hadi Sh1,866, wakati dizeli ikipanda kutoka Sh1,672 hadi Sh1,695.
Hii ni mara ya pili katika miezi miwili kwa Ewura kupandisha bei ya bidhaa hizo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Ewura ilisema kuwa bei hizo ni elekezi kwa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine, na zitaanza kutumika kuanzia leo Jumatano, Mei 6, 2015.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote, petroli, dizeli na taa, zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la Aprili 1, 2015.
Kulinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla kwa petroli na dizeli pia zimeongezeka kwa, Sh110.85 kwa lita sawa na asilimia 6.72, Sh22.94 kwa lita ya dizeli sawa na asilimia 1.46 wakati bei ya mafuta ya taa imeshuka kwa Sh30.70 kwa lita sawa na asilimia 1.98.
Taarifa ya Ewura ilisema kuwa mabadiliko hayo yametokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.
“Kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.
“Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya uamuzi stahiki kuhusu ununuzi wa bidhaa za mafuta,” inasema taarifa ya Ewura.

No comments:

Post a Comment