Na Waandishi Wetu, , Mwananchi
Posted Ijumaa,Mei8 2015 saa 8:50 AM
Posted Ijumaa,Mei8 2015 saa 8:50 AM
KWA UFUPI
- Mvua hiyo iliyofikia kipimo cha milimita 132.5 kwa mujibu wa vipimo vilivyofanywa katika kituo cha Shule ya Msingi ya Maktaba, ilisababisha barabara kujaa maji na nyingine kuharibika na madaraja kadhaa kukatika.
Dar es Salaam. Mvua kubwa iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo tangu juzi imesababisha vifo vya watu watano huku mamia wakikosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa.
Mvua hiyo iliyofikia kipimo cha milimita 132.5 kwa mujibu wa vipimo vilivyofanywa katika kituo cha Shule ya Msingi ya Maktaba, ilisababisha barabara kujaa maji na nyingine kuharibika na madaraja kadhaa kukatika.
Mkurugenzi Mkuu wa Hali ya Hewa, Dk Agnes Kijazi alisema jana kwamba kipimo hicho cha mvua ni cha juu mno kulinganisha na kile cha wastani ambacho ni kati ya milimita 16 na 30.
“Kwa takwimu za mwezi Mei, kiwango hiki hakijawahi kufikiwa kwa miaka 10 iliyopita.” Alipotakiwa kufafanua miezi mingine, Dk Kijazi alisema hakuwa na takwimu kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
Awali, Dk Kijazi alitoa taarifa ikisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa “hali ya mvua inatarajiwa kuendelea katika baadhi ya siku hadi Mei 20, mwaka huu”.
“Mamlaka inaendelea kushauri wakazi wa maeneo hatarishi pamoja na watumiaji wa bahari kuchukua tahadhari,” alisema Dk Kijazi.
Watano wafa
Kutokana na mafuriko hayo, watu watano wakiwamo watoto wawili, walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema waliopoteza maisha ni watoto wawili na mzee mmoja ambao majina yao hayajafahamika.
“Mtoto mmoja (2) alisombwa na mafuriko katika eneo Machimbo ya Makangarawe na mzee mmoja alifariki jana baada ya mvua kunyesha na kujaa ndani ya nyumba yake. Mtoto mwingine ambaye bado hajapatikana alisombwa na mafuriko pia,” alisema Sadick.
Hata hivyo, habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zilisema kuwa waliopoteza maisha ni watu watano.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alimtaja mtu aliyefariki dunia kuwa ni Shabani Idd (73) mkazi wa Manzese.
No comments:
Post a Comment