Monday, 24 December 2018

Maandamano Sudan: Polisi wakabiliana na wapenzi wa mpira wa miguu wanaompinga Omar al-Bashir

demonstration in Atbara on 20 Dec
Polisi nchini Sudan wamewatimulia mabomu ya machozi mashabiki wa mpira mabao walikuwa wakiandamana kutaka kung'atuka kwa rais Omar al-Bashir.
Maandamano yaliyoanza wiki iliyopita yametanda nchi nzima huku waandamanaji wakitaka kuondoka kwa raisi huyo aliyedumu madarakani kwa miaka 29.
Mamia ya waandamanaji walizuia barabara moja iliyokaribu na uwanja wa mpira katika mji mkuu wa Khartoum, siku ya Jumapili kisha kukabiliana na polisi wa kutuliza ghasia.
Viongozi wa upinzani wanadai watu 22 wameuawa toka Jumatano ya wiki iliyopita, lakini viongozi wa serikali wanadai idadi hiyo imetiwa chumvi.
Maandamano hayo yalilipuka baada ya kuongezeka kwa bei ya mafuta mkate. Lakini sasa yamechukua sura mpya ya kutaka uongozi wa Bwana Bashir ufikie tamati.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita bei ya baadhi ya bidhaa muhimu zimeongezeka mara mbili nchini Sudan huku mfumuko wa bei kufikia asilimia 70.
Thamani ya sarafu ya nchi hiyo imeporomoka mara dufu na tayari kuna uhaba wa pesa katika miji mikubwa kama Khartoum.
Madaktari nao wamejitosa katika maandamano hayo leo Jumatatu ili kuongeza shinikizo dhidi ya Bashir shirika la habari la Associated Press limeripoti.
Bashir alichukua hatamu za uongozi katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwaka 1989.

No comments:

Post a Comment