Wasanii nyota wa Tanzania Diamond Platnumz na Rayvanny sasa ruksa kufanya maonesho yao ya nje ya Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limeeleza kuwa wasanii hao wapo huru kufanya maonesho yao ya nje ya nchi, huku marufuku ya kutumbuiza ndani ya Tanzania ikisalia.
Diamond na wasanii kutoka kundi analolimiliki la Wasafi wanatarajiwa kupanda jukwaani mjini Embu Disemba 24, kisha jiji la Mombasa mnamo Disemba 26 kabla ya kuhamia visiwani Komoro ambapo watatumbuiza Disemba 28.
Mkesha wa mwaka mpya nyota hao watatumbuiza katika viwanja vya bustani ya Uhuru jijini Nairobi ambapo wataungana na kundi maarufu la muziki kutoka Jamaica la Morgan Heritage.
Wasanii hao waliomba radhi wiki iliyopita kabla ya kuelekea Kenya huku Diamond akiwaambia wanahabari jijini Nairobi kuwa mamlaka za Tanzania zilimruhusu kwenda Kenya kutumbuiza. Basata hata hivyo ilikana kupokea taarifa rasmi ya kuomba radhi na kuwafungulia nyota hao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na kutiwa saini na katibu mkuu wa Basata Godfrey Mngereza imesema kuwa ruhusa imetoka baada ya kikao kilichoketi leo na kujadili maombi yao kuomba kusamehewa huku moja ya jambo walilolibaini ni kwamba wasanii hao walikuwa wameshaingia mkataba wa kufanya maonesho hayo kabla ya kupewa adhabu.
"...Kwa kuzingatia mahusiano mazuri kati ya nchi yetu na nchi nyengine lakini pia kuzingatia athari kwa mashabiki wa nchi hizo ambao tayari walishakata tiketi za maonyesho hayo, Basata imewaondolea katazo la maonesho hayo ya nje na kubakiza katazo la ndani ya nchi mpaka pale Diamond na wenzake watakapoonesha mabadiliko chanya kitabia," imesema taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment