
Diamond Platnumz na Rayvanny wamefungiwa kufanya onyesho lolote ndani na nje ya Tanzania na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Baraza hilo limesema marufuku hiyo ya muda usiojulikana inaanza kutekelezwa leo.
Wasanii hao wawili walikuwa awali wametakiwa kuuondoa wimbo wao kwa jina 'Mwanza' kutoka kwenye mitandao ya kijamii, lakini wimbo huo umeendelea kuwepo kwenye YouTube.
Aidha, wameendelea kuucheza kwenye matamasha.
"Baraza limefikia maamuzi ya kuwafungia rasmi kutokana na wasanii hawa kuendelea kuonyesha dharau na utovu wa nidhamu kwa mamlaka zinazosimamia masuala ya sanaa nchini na uvunjifu wa maadili uliokithiri unaofanywa na waandaaji wa Tamasha la Wasafi 2018, chini ya uongozi wake Diamond Platnumz," taarifa ya Basata ambayo imetiwa saini na Onesmo Kayanda kwa niaba ya Katibu Mtendaji inasema.
"Pamoja na maelezo hayo, Baraza linatoa taarifa kuwa kibali cha Tamasha la Wasafi 2018 kimesitishwa kutokana na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu katika uendeshaji wa tamasha hilo hapa nchini."

Baraza hilo wakati huo liliwaonya wasanii waliohusika, Rayvanny na Diamond, pamoja na uongozi wa Wasafi Limited kufuata sheria na "kutoutumia wimbo huo na nyimbo nyingine zilizofungiwa kwa namna yoyote ile."
Baraza hilo liliwataka "kuuondoa wimbo huo mara moja kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kufika saa kumi kamili" siku hiyo.
Taarifa hiyo ilitiwa saini na Katibu Mtendaji wa Basata Godfrey Mngereza.
No comments:
Post a Comment