Ndege mpya ambayo imekuwa ya karibuni zaidi kununuliwa na serikali ya Tanzania kwa ajili ya kutumiwa na Shirika la Ndege la Air Tanzania imewasili Dar es Salaam.
Ndege hiyo, ambayo imeundwa na kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Airbus, ni ya muundo wa A220-300.
Ndege hiyo itakuwa na jina la Dodoma, mji mkuu rasmi wa Tanzania. Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa kuhamishia shughuli zake zote jijini Dodoma.
Tanzania iliponunua ndege ya majuzi zaidi, 787-8 Dreamliner ya kampuni ya Boeing, ndege hiyo ilipewa jina la Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika.
- Mambo makuu aliyoyasema Magufuli akipokea Dreamliner
- Magufuli: Tutarejeshewa sehemu ya anga iliyopewa Kenya
Sawa na ndege hiyo ya Dreamliner, ndege hiyo mpya ya Airbus ina nembo ya 'Hapa Kazi Tu' chini ya jina Dodoma.
Hapa Kazi Tu imekuwa kauli mbiu ya Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli tangu wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015.
Kampuni ya Airbus Alhamisi iliandika ujumbe kwenye Twitter: "Kiwango cha joto ni chini ya sifuri hapa Mirabel, Canada lakini twiga kutoka Kilimanjaro huwa hawaingiwi na wasiwasi kutokana na baridi! Tunazindua rangi mpya za #A220 za @AirTanzania, ambao karibuni watakuwa shirika la kwanza la Afrika kuwa na ndege aina ya A220.
Mirabel ni kisiwa kinachopatikana eneo la Montreal, kusini mwa Quebec ambapo zinapatikana karakana za Airbus.
Airbus A220-300 ndiyo Bombardier?
Ndege za Airbus A220 zilikuwa zinafahamika kama Bombardier CS100s kabla ya Airbus kuununua mradi huo wa utengenezaji wa ndege za C Series.
Ununuzi huo ulifanikishwa kupitia mkataba wa kibiashara kati ya kampuni ya Airbus na kampuni nyingine mbili: Bombardier Inc na Investissement Québec ambao ulianza kutekelezwa 1 Julai, 2018.
Airbus sasa humiliki 50.01% yahisa katika ubia wa utengezezaji wa ndege hizo ambao kirasmi hufahamika kama C Series Aircraft Limited Partnership, huku Bombardier na Investissement Québec wakimiliki takriban 34% na 16% ya hisa mtawalia.
Makao makuu ya mradi huo wa utengenezaji wa ndege pamoja na karakana zake vyote vinapatikana Mirabel, Québec.
Kutokana na ushirikiano huo, na hali kwamba Airbus inamiliki hisa nyingi, mradi wa C Series huhesabiwa sasa kuwa chini ya Airbus.
Mambo muhimu kuhusu Airbus A220-300
Ndege hii urefu wake ni mita 38.7, na kwa jumla inaweza kuketi abiria 141.
Urefu wake kutoka chini kwenda juu ni mita 11.5, na upana wa mabawa yake ni mita 35.1.
Airbus 220-300 inaweza kusafiri umbali wa 5,920km safari moja, na inaweza kupaa ikiwa na uzani wa tani 67.6, na kutua ikiwa na uzani wa tani 58.7.
A220-300 ndiyo ndege kubwa miongoni mwa ndege za familia ya A220 na iliundwa kulenga soko la safai za ndege zinazowabeba abiria kati ya 130-160.
Ni ndege ambayo imeundwa kupunguza gharama ya matumizi yake ya mafuta kwa kila safari na pia kuwa yenye uwezo wa juu.
Injini zake zimepunguza matumizi ya mafuta kwa kila abiria kwa asilimia 20 ukilinganisha na ndege za awali za aina yake.
Ndege za A220 zimejengwa kwa vipande vinavyoweza kutengenezwa kwa haraka kiwandani iwapo vitahitajika wakati wa ukarabati.
Injini zake pia huwa za familia moja. Marubani waliozoea ndege aina ya A220-300 na A220-100 hawahitaji mafunzo zaidi kuweza kuziendesha.
Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege ya aina gani?
Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege ya kisasa ambayo hutumia injini ya kisasa zaidi aina ya Trent 1000 TEN. Bei yake inakadiriwa kuwa $224.6 milioni.
Injini hiyo inatumiwa katika ndege zote mpya aina ya Boeing 787 na huhifadhi mafuta, ambapo huwa inachoma mafuta kwa kiwango cha asilimia tatu chini ukilinganisha na ndege za aina hiyo na kuyatumia vyema zaidi.
Hilo huiwezesha kupunguza matumizi ya mafuta ukilinganisha na ndege nyingine za ukubwa kama wake kwa asilimia 20-25, aidha hupunguza utoaji wa gesi chafu kwa kiwango sawa na hicho.
Aidha, huwa haipigi kelele sana. Ni ndege ambayo imechukua uwezo na kasi ya ndege kubwa aina ya 'jet' na kuuweka kwenye ndege ya ukubwa wa wastani.
Ina uwezo wa kubeba abiria 262 ni ya kisasa zaidi kuwahi kumilikiwa na serikali ya Tanzania. Mataifa mengine kama vile Kenya na Ethiopia hata hivyo yamenunua ndege kama hizo kadha.
- Ndege kubwa zaidi zilizowahi kuundwa duniani
- Ndege ya kwanza iliyoundwa China yapaa
- China yazindua meli kubwa ya kivita
Ndege hii ina uwezo wa kusafiri kilomita 13,620 kwa wakati mmoja na urefu wake ni mita 57. Upana wa mabawa yake ni mita 60. Urefu wake kutoka chini hadi juu ni mita 17.
Ethiopia ilikuwa nchi ya kwanza duniani kando na Japan kuanza kutumia ndege aina ya Boeing 787-8 Agosti 2012.
Air Tanzania ina ndege ngapi?
Shirika la Air Tanzania kwa sasa lina ndege saba, baada ya kununuliwa ndege sita chini ya mpango wa kufufua shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1977.
Kuna Bombardier DASH8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika Tanzania Septemba 2016 na moja Juni 2017; Bombardier CS300 mbili na Boeing 787 Dreamliner ambazo zilitua Tanzania kati ya mei na Julai 2018.
Shirika hilo lilikuwa na Bombardier DASH8 Q300 moja ambayo ilikuwa ikihudumu tangu 2011.